15 Septemba 2025 - 23:39
Source: Parstoday
Iran yapinga madai ya G7, na kuyataja kuwa ya uongo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekanusha vikali tuhuma zilizotolewa katika taarifa ya pamoja ya G7 na washirika wake, ikizitaja kuwa ni za kupotosha, zisizo na msingi, na ni mbinu ya kisiasa ya kujiepusha na lawama.

Wizara hiyo imesisitiza kuwa kueneza tuhuma za uongo dhidi ya wale wanaolinda usalama wa taifa la Iran ni kupotosha ukweli kwa makusudi, na ni mbinu ya hila ya kuhamisha lawama kutoka kwa wale wanaojihusisha na vitendo haramu na vya kuleta machafuko duniani, hususan katika eneo la Asia Magharibi.

Iran imesema kuwa Marekani na wanachama wengine wa G7 wanapaswa kuwajibika kwa mchango wao katika kuvuruga usalama wa kikanda na wa kimataifa—hasa kwa kushirikiana na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa, sheria za kibinadamu, na haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Israelkatika ardhi ya Palestina iliyokaliwa kwa mabavu, pamoja na kuunga mkono makundi ya kigaidi.

Wizara hiyo ilisema: “Wakati ambapo utawala wa Kizayuni, kwa msaada kamili kutoka Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, na wadhamini wengine wa taarifa hii ya chuki dhidi ya Iran, unatekeleza mauaji ya halaiki na jinai za kimbari katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kuchochea vita vinavyoendelea katika ukanda huu, kutoa taarifa dhidi ya Iran ni jaribio la kuondoa macho ya dunia kutoka kwenye jinai ya karne hii na ushiriki wa wazi wa mataifa haya.”

Taarifa hiyo ilihitimisha kwa kusema kuwa badala ya kuendeleza mbinu za kutafuta mchawi zinazotokana na fikra za kikoloni na ubaguzi wa kimadaraka, wadhamini wa taarifa hizo zisizo na uwajibikaji wanapaswa kurekebisha sera zao potofu na za jinai dhidi ya Iran na ukanda mzima.

Your Comment

You are replying to: .
captcha